Kamanda Simon Sirro: Bodaboda marufuku kuegeshwa kwenye vituo vyao maalumu kwa ajili ya kusubiri abira baada ya saa 6:00 usiku
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam juzi, Kamanda wa jeshi hilo kanda maalumu ya Dar es
Salaam, Simon Sirro, alisema kuwa kuanzia sasa, ni marufuku kwa bodaboda
kuegeshwa kwenye vituo vyao maalumu kwa ajili ya kusubiri abira baada ya muda
huo, lengo likiwa ni kuimarisha usalama wao na watu wengine jijini Dar es
Salaam.
Akifafanua, Kamanda Sirro alisema kuwa wamelazimika kutoa agizo hilo
baada ya kubaini kuwapo kwa matukio mengi ya uhalifu yanayohusisha uporaji wa bodaboda
kutoka kwa madereva hao nyakati za usiku. Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, haingii
akilini kwa madereva wa bodaboda kuendelea kukaa kwenye vijiwe wakisubiri
abiria usiku kucha ilhali ikifahamika wazi kuwa baada ya saa 6:00 usiku huwa
hakuna abiria wa kuwasubiri hasa kutokana na ukweli kuwa watu walioko kwenye
maeneo ya starehe kama baa huwa tayari wameshaondoka baada ya maeneo hayo
kufungwa kila inapofikia mida hiyo.
Siyo nia yetu kuzungumzia kwa undani juu ya
agizo hilo. Bali, tunatambua kuwa kwa ujumla wake, lengo la Polisi katika kanda
maalumu ya Dar es Salaam ni kuhakikisha kuwa mara zote, usalama wa raia na mali
zao unabaki kuwa wa uhakika. Hata hivyo, jambo pekee tunalodhani kwamba ni
vizuri likazingatiwa kwa umakini ikiwa utekelezaji wa agizo hilo utaanza ni
kuona kuwa busara inatangulizwa. Kwamba, badala ya kuanza kutumia nguvu kungali
mapema kwa nia ya kushinikiza utekelezaji wa ratiba hiyo, ni vyema polisi
wakatoa elimu ya kutosha kwa wahusika ili kuepusha rabsha zinazoweza
kujitokeza.
Madereva wa bodaboda waelezwe ni kwa nini kuanzia sasa hawaruhusiwi
kuwa kwenye vituo vyao wakisubiri abiria usiuku wa manane. Waelezwe kwa kina ni
kwa namna gani utekelezaji wa agizo hilo utaimarisha usalama kwao na kwa jamii
inayowazunguka. Kwa mfano, ni vizuri madereva wa bodaboda wakaelezwa namna
wanavyoweza kupata matatizo pale wahalifu watakapowapora pikipiki zao nyakati
za usiku na kwenda kuzitumia katika matukio ya ujambazi. Waelezwe kwambva
katika matukio ya aina hiyo, ikiwa pikipiki husika itakamatwa, ni wazi kwamba
watakaosumbuka na hata kuwekwa ndani wakati uchunguzi ukiendelea ni pamoja na
wao wenyewe. Aidha, jambo jingine muhimu kuzingatia kungali mapema ni kwa jeshi
la polisi kufafanua kwa uwazi kuwa kinachozuiwa ni madereva wa bodaboda kukaa
vijiweni kwao usiku wa manane wakisubiri abiria.
Isije kuonekana kuwa baadhi ya
askari wakitafsiri vibaya agizo hilo kwa kuwasumbua watu wanaoendesha pikipiki
barabarani nyakati za usiku baada ya saa 6:00. Ni kwa sababu, kwa mujibu wa
Kamanda Sirro, kinachokatazwa ni madereva wa bodaboda kukesha vijiweni mwao
wakisubiri abiria. Ni imani yetu kwamba hakuna dereva wa pikipiki
atakayekamatwa akiwa barabarani kwa tuhuma za kukiuka agizo la kutokaa vijiweni
baada ya saa 6:00 usiku